Ado Shaibu : “Sijaona hoja yoyote ya maana ya kunifanya niondoke ACT”
Monday, December 11, 2017
Ado Shaibu : “Sijaona hoja yoyote ya maana ya kunifanya niondoke ACT”
Ikiwa vuguvugu la kuhama kwa wanasiasa limepamba moto nchini, Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, amesema haoni hoja ya msingi itakayo mshawishi kukihama chama hicho.
Ado aliyasema hayo Novemba 9, 2017 siku moja baada ya aliyekuwa Mgombea kiti cha Urais kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kupitia ACT ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa chama hicho, Mama Anna Mgwira kuhamia CCM, uamuzi alioutangaza kwenye Mkutano wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) uliofanyika mjini Dodoma.
Ado alifunguka kuwa, katika kipindi cha wiki mbili zilizopita ambacho hakuwepo kwenye mitandao ya kijamii na kupatikana kwenye simu iliyozoeleka, kuna baadhi ya watu baada ya kurejea hewani, walimtumia jumbe zenye kuhoji kama ameshahamia CCM kutoka ACT.
“Jibu langu kwao lilikuwa jepesi. Siasa halisi si mzaha Kama mchezo wa komborera. Kwamba Leo ujifiche hapa kesho pale Kisha ubutue. Siasa ni itikadi. Siasa ni falsafa. Siasa ni sera. Siasa ni hisia za watu waliokuamini na kukuheshimu. Ukiheshimu Itikadi, falsafa, sera na hisia za watu waliokuheshimu na kukutumaini ndani na nje ya chama, hauwezi kuhama hovyo Kama wacheza komborera wanavyobadili maficho yao,” alisema na kuongeza.
“Kuhama Chama ni lazima kusukumwe na hoja za msingi na zenye mashiko. Kwa sasa, sijaona hoja yoyote ya maana ya kunifanya niondoke Act Wazalendo.”
Siku za hivi karibuni kumekuwepo na wimbi kubwa la wanasiasa wa vyama vya upinzani kuhamia chama Tawala CCM kwa madai ya kumuunga mkono Rais John Magufuli kutokana na kuridhishwa na utendaji kazi wake, miongoni mwao wapo waliokuwepo Wabunge, madiwani, viongozi kwenye vyama vya upinzani na wanasiasa mashuhuli.
Comments
Post a Comment