Serikali Yasaini Mikataba Minne Ya Ujenzi Wa Barabara kilomita 402 za Lami
Tuesday, December 12, 2017
Serikali Yasaini Mikataba Minne Ya Ujenzi Wa Barabara kilomita 402 za Lami
Serikali imesaini mikataba minne na kampuni nne za ujenzi wa barabara yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 702 kwa ujenzi wa kilomita 402.
Tukio hilo la kusaini mikataba hiyo limeshuhudiwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Mandeleo ya Afrika (AfDB), MarieHellen Minja, wabunge ambao miradi hiyo ya Barabara itapita majimboni mwao, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na wakandarasi walioshinda zabuni.
Akizungumzia utiaji saini huo, Waziri Mbarawa amesema fedha hizo zitatumika katika ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Tabora (Usesula)- Koga hadi Mpanda yenye urefu wa kilomita 335 na kilomita 67 kutoka Mbinga hadi Mbamba Bay mkoani Ruvuma.
Waziri Mbarawa amesema ujenzi wa barabara hizo ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), na ahadi za Rais John Pombe Magufuli wakati wa kampeni.
Aidha, Waziri Mbarawa ametumia nafasi hiyo kuwataka wakandarasi walioshinda zabuni kujenga barabara zenye ubora na viwango kwa kuzingatia muda wa ujenzi.
Profesa Mbarawa ameongeza kuwa nia ya Serikali ni kuona ujenzi wa barabara hiyo unakamilika kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
“Naomba TANROADS msimamie ujenzi wa barabara yenye ubora kwani wakandarasi wengi ni wajanja na ikitokea mtu ameharibu asipewe nafasi kabisa ya ujenzi wa barabara hapa nchini,” amesema Waziri Mbarawa.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale, amesema kuwa wakandarasi waliopewa kazi wametokana na uchambuzi mkubwa uliofanyika kati ya wakandarasi 129 waliojitokeza mwaka 2016 kuomba zabuni za ujenzi wa barabara hizo.
Mhandisi Mfugale amefafanua kuwa ili kurahisisha ujenzi wa barabara hizo wamegawa kwa wakandarasi wanne ambapo barabara ya Usesula hadi Komanga kilomita 108 itajengwa na Kampuni ya Jiangxi Geo-Engineering Group Corporation Limited ya China kwa gharama ya zaidi ya Sh.Bilioni 158 na itajengwa kwa miezi 36.
“Komanga hadi Kasinde kilomita 108 itajengwa na Mkandarasi Kampuni ya China Wu Yi Co. Limited kwa zaidi ya sh.billioni 140 na Kasinde hadi Mpanda kilomita 105 Mkandarasi Kampuni ya China Railway Seventh Group Co.Ltd kwa sh. Bilioni 133,” amesema Mhandisi Mfugale.
Mhandisi Mfugale ameongeza kuwa barabara ya Mbinga hadi Mbamba Bay kilomita 67 inajengwa na Mkandarasi China Henan International Corporation Group Co.Ltd (Chico) kwa sh. Bilioni 129.
Amesema TANROADS imejipanga kusimamia ujenzi huo kwa kufuata viwango vinavyohitajika vya ujenzi wa barabara nchini.
Mwakilishi Mkazi wa AfDB, Bi. Minja amesema ofisi yake itaendelea kutoa mchango kwa serikali katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchini pale watakapo hitajika.
Bi. Minja amesema kuwa matarajio ya AfDB ni kuona Tanzania inapata maendeleo kwa haraka na njia rahisi ni kupitia miundombinu.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe ambaye barabara ya Tabora hadi Mpanda inapita jimboni kwake ambapo amesema kuwa ujenzi huo utafungua fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, amesema barabara hiyo itakuwa kiungo muhimu kati ya Tanzania, Msumbiji na Malawi.
Amesema kuwa Nyasa ina vivutio vingi vya utalii hivyo ujio wa barabara hizo utakuwa njia rahisi ya kuwafikisha watalii eneo hilo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Comments
Post a Comment